Nini Siyo Sunna

Je sunna ni ndevu, masharubu, nguo, kilemba, au muonekano wa mavazi?

Hivi nini yawezekana kuwa ndiyo Sunna ya Rasulullah?

Sunna ya Allah yani SUNNATILLAH ni nini?

Wenye ufahamu mdogo wanajua sunna kuwa ni operesheni wanayofanyiwa watoto wa kiume.

Ufahamu wa sunna wa wenye ufahamu wa wastani ni mpana kidogo... Kwao, sunna ni Ndevu, masharubu na mavazi!... Kwao, kumfuata Rasulu wa Allah ni kujitumbukiza katika mavazi ya miaka 1400 iliyopita; kufuata mila na desturi za kipindi hicho!..

Hawa ni waislam wenye kusema kwamba wao ndiyo waislamu na wale wenye kuvaa mashati ya mikono mifupi si waislamu!

Hawa ni kama waislamu waliomuua Kiongozi wa Uwalii, Mlango wa elimu Hazrat Ali!... Ufahamu wao, ni ufahamu uliomuona huyu swahaba mkubwa ametoka nje ya dini!.

Tafitini yaliyosemwa na Hazrat Muhammad alayhissalaam kuhusu Hazrat Ali... Muelewe hali na kiwango cha ufahamu wa waislamu ambao walimuona yu nje ya njia ya Rasulullah!

Watofautisheni ambao, kwa madai ya kuhudumia dini na sunna wamefanya dini ufalme na wamekuwa wakiitumia DINI kutawala watu.

Nimeamua nilifafanue jambo hili wazi wazi baada ya kuona habari kwenye ukurasa wa internet ulionukuu ufafanuzi nilioufanya!

Nawaomba mfikirie vizuri nitakayoyaeleza...

Nilipokuwa na miaka 20 yani  miaka 40 iliyopita, nilimuota Rasulullah akaniambia niende kwa Hazrat Abubakar... Kilichofuata si muhimu hapa... Na mimi baadae mwaka huo nikaandika maisha ya Hazrat Abubakar... Baadae nikaandika kidogo maisha ya Hazrat Rasulallah ya kipindi cha Makka kwa kuambatanisha na hadithi katika kitabu nilichokiita “Muhammed Mustafa” alayhissalam.

Nimeandika haya kwa sababu ifuatayo. Nilitafiti kwa undani sana maisha ya wakati huo... Nilisoma karibu Hadithi 60 sahihi.

Kama inavyojulikana Rasul wa Allah Muhammed Mustafa alayhissalaam alizaliwa ndani ya kabila la Kureishi lililokuwa na upapatikiaji wa Masanamu... Babu, na ndugu zake wengine walikuwa wenye kufuata taratibu za kabila...

Rasulullah akakulia humo... ALIVAA kama wao, ALIACHA NDEVU kama wao, ALIFUNGA KILEMBA kama wao!. Alikaa, kusimama, kula na kunywa kama wao...

Aliendelea hivyo mpaka alipofikisha miaka 39 akawa Rasulu wa Allah!...  Kama Rasulu wa Allah alibaini ukweli katika umri huu; Ulipokamilika UNABII miaka mitatu baadae, akaanza kuwafahamisha watu yakufanya kwa mujibu wa Wahyi aliopata, ili wajichumie kwa ajili ya maisha yao ya milele.

HAKUBADILI NDEVU WALA MAVAZI YAKE katika kipindi hiki wala baada yake!

Aliendelea kufunga kilemba kama wao, alivaa kama wao, na kuzunguuka na ndevu kama wao!. Hata ile nguo yake yenye rangi nyingi na bakora yake aliendelea nayo!..

 Sunna ya Rasulu wa ALLAH ni sunna ya makusudio ya jina “ALLAH” ambaye ndiye Rasulu wake; “SUNNATILLAH”!.

Hata sisi tukiielewa “SUNNATILLAH” na kuifuata tutakuwa tumeifuata sunna ya Rasulullah na tutakuwa kwenye “SUNNATILLAH”! Lakini si kwa ndevu, masharubu, nguo na vilemba!

VILEVILE JAMBO MUHIMU LINALOBIDI LIBAINIKE NI:

Rasulullah hakuingilia wala kuwashauri kuhusu mavazi na desturi wapapatikia masanamu wakina Abu Jahil, Abu Lahab na mfuwasi wao ambaye alimuua mjukuu wa Rasulullah, Yazid; Aliendelea kuwa ni mwenye kuvaa kama wao. Kwa sababu hili halikuwa na umuhimu katika kufanikisha yanayotakikana na DINI; na wala halina uhusiano na ukweli wa maisha ya milele au kujulikana kwa makusudio ya jina “ALLAH”

Na hii inamaanisha kwamba...

ALLAH akimuongoza mtu, mtu huyu anaweza akaendelee kuvaa kwa mujibu wa mila na desturi za jamii yake, lakini hatofuata jamii yake katika mambo yanayohusika na “SUNNATILLAH”; Na ataendelea kuufahamisha ukweli aliojifunza unaohusika na uongofu alioupata!.

Hii inamaanisha, si kupinga mila na desturi katika mambo kama mavazi, bali kuendelea nayo ndiyo SUNNATIRASUL!.

Kwa sababu DINI haikuja kwa ajili ya mapinduzi ya muonekano wa mavazi ya watu! Si kazi ya Dini kushughulika na muonekano wa mavazi. Kwa mujibu wa suna, watu wana haki ya kuvaa, kusoma, kuishi, na kufanya kazi kufuatano na imani zao bila kuharibu amani ya jamii! Hata kama hili litakuwa liko kinyume kwa wale ambayo mbongo zao hazijaelewa!

Kutoa hukumu juu ya dini ya mtu kwa kuangalia mavazi yake ni ishara tosha ya mtu asiyeendelea mwenye ubongo wenye kufuata mkumbo.

Rasulu wa kusidio la jina “ALLAH”, kwa kuwafahamisha watu ukweli wa utaratibu na mfumo wanaoishi ndani yake, alijitahidi kuwafanya waishi kwa mujibu wa mfumo na utaratibu wa ALLAH ambao ulipewa jina la “DINI”, na hivyo basi kuwa wenye kujiandaa na maisha ya milele!

“MTU WA DINI” ni yule aliyetafiti, kuuliza na kuuelewa utaratibu na mfumo wa ALLAH na kukubali kuishi kwa mujibu wake!. MTU WA DINI kutokana na mfumo huu aliouSOMA anakuwa “MUTTAQI” yani mwenye kuchukua tahadhari dhidi ya hatari zinazokuja alizozibaini!.

Kufuata sunna ya Rasulu wa Allah maana yake ni kuuthamini ufahamu wake, kudumu katika njia aliyoionyesha na kwa kufanya aliyosema kufikia mambo mazuri yanayokuja. Maana yake ni kuuvumbua uhakika wa kiini chake; na kufanikisha matokea yake ya kusisimua!. Sio kufuja maisha kwa kufuata mkumbo.

Kufuata sunna ya Rasulu wa Allah maana yake ni kuchanga na watu bila malipo elimu aliyozawadiwa. Siyo kuwaliwaza watu na riwaya za muonekano wa mavazi!.

Mtu aliyeuelewa mfumo na utaratibu wa Allah yani “SUNNATILLAH” na kisha akafanywa yanayopaswa anakuwa ndiyo mtu aliyefuata “SUNNATIRASULULLAH”!.

Onyo la kwamba “Atakayejifananisha na kundi lolote basi atakuwa miongoni mwao” linamaanisha kwamba mtu yupo katika jumuia ambayo anachangia nayo Fikira na Imani... na si ufanano wa mavazi au  ndevu!.

Kama tulivyo eleza katika makala yetu yenye kichwa “Kutawala watu kwa kutumia dini”, kuna baadhi ya watu wamepiga marufuku udadisi na utafiti wa DINI; na hivyo basi wamepelekea ukuaji wa watu wenye mbongo kama kaseti, wenye kuiga na wasio na uwezo wa kufikiri.

Dunia ni pahala pa hekima na kila ufafanuzi wa Rasulullah umelala kwenye hekima fulani!. Mtu mwenye akili ni yule mwenye kuuliza na kutafiti kila jambo ili kumuelewa vizuri Rasulullah na kujaribu kuifikia hekima ya lililofundishwa.

Hili limeashiriwa na onyo la kwamba “hekima ni kitu kilichopotezwa na mumin

Yeyote aliye na mgongano wa mawazo au mapengo katika mfumo wake wa kufikiria, ni mfuata mkumbo ambaye hajailewa dini na hajaweza kuuSOMA ufanyajikazi wa utaratibu na mfumo aishio ndani yake.!.

Ukweli ni kwamba  DINI haikubali ufuataji mkumbo!.

Kuiga matendo kunazaa matokeo yanayofanana; lakini hili haliwezekani kwa kuiga mawazo !.

Kuwa “Faqih” yani mwenye ueleo, ni Lutufu(upendeleo) ya Allah. Hivyo mtu anaacha kuwa mwenye kufuata mkumbo. Hata siku moja kukumbuka kanuni za FIQIH hakumaanishi kuwa “FAQIH”.

Uwezo wa kuhifadhi vitu kichwani umepoteza thamani baada ya uvumbuzi wa kaseti!.

Dini imefahamishwa kwetu kuwa ni yenye kustahili kusomwa ili ubaini utaratibu na mfumo unaoishi ndani yake; la muhimu zaidi “UJIFAHAMU MWENYEWE” ! Uivumbue hazina iliyo katika uhakika wako; Na mwisho ufahamu kusudio la jina ALLAH kwa mujibu wa elimu ya holografia na kuijua nafasi yako katika ulimwengu.. Wale ambao hawajalielewa hili katika maisha yao hawajaisoma “IHLAS” Hata kama wameirudia mara laki!...

Tulifikirie vizuri onyo la Rasulullah kwamba, “Kuna mwenye kuswali sana lakini hajaambulia lolote isipokuwa uchovu; kuna mwenye kufunga sana lakini zaidi ya njaa hajapata  faida yoyote”

Rasulu wa Allah ametufahamisha Quran ili tuielewe na kutafakari. Tufanye hivyo hadi ufike wakati ambao hatua zote tunazochukua maishani ziwe zenye kuwiana na SUNNATILLAH! Tusizungumze kipuuzi juu ya nywele, ndevu, mavazi, Rasulu hakuja ili tupoteze umri kwa hukumu zinazohusu watu.

Je ni upi ufahamu wa dini unaoingilika kwa kusema kwamba hakuna mungu wala wazo la uungu pamoja na Kusudio la jina ALLAH. (La ILAHA ILLA ALLAH)?

Wanaofuja umri wao kwa kuiga bila kudadisi wala kujaribu kuelewa hili; watapigwa na bumbuwazi na kupata majuto makubwa kama matokeo ya kushindwa kuisoma hazina.

Inasikitisha kwamba ndani ya huu mfumo hakuna wazo la kufidia!.

Tahadhari: Huu ni mtazamo wangu binafsi; Haumlazimishi yeyote yule kuufuata; Apendae atachangia, asiyependa hatochangia. Kuna baadhi ya watu, kutokana na kuwa tofauti na matarajio yao wanadai kwamba tunachanganya vichwa na wanapiga marufuku tusisomwe kwa kusema kwamba “tunawafanya watu wafikirie na hivyo tupigwe marufuku”.

AHMED HULUSI
19 May 2005
NC, USA